MUHADHARA MUHIMU ALIO UTOA MHESHIMIWA SAYYID SWADIQ SHIRAZI PINDI ALIPO KUTANA NA KIKUNDI CHA WANAFUNZI WA KIAFRIKA NA MAZUNGUMZO YAKE YALIHUSIANA NA ULAZIMA WA KUFUATA NYENDO ZA MTUME MTUKUFU (S.A.W.W)

Kikundi cha wanafunzi wa elimu ya kidini wa kiafrika walifanya ziara ya kumtembelea kiongozi wa juu wa kidini mheshimiwa Ayatullahil-udhmaa Sayyid Swadiq Al-huseiniy Al-shiraziy mnamo tarehe kumi na saba 17 ya mwezi wa Rabiul-awwal (mfungo sita) mwaka 1427 hijiria nyumbani kwake katika mji mtukufu wa Qum, na katika ziara hiyo mheshimiwa alitoa katika mkusanyiko huo maneno yake muhimu na kati ya maneno aliyo yasema ni haya yafuatayo:
Ninamuomba Mwenyezi Mungu mtakasifu na mtukufu kwa fadhila zake zenye kutuenea na pana katika usiku huu wenye baraka ambao tunasherehekea kumbukumbu ya mazazi ya bwana wa wamwanzo na wamwisho, bwana wetu na kiongozi wetu Abil-qaasim Muhammad (s.a.w.w), na kumbukumbu za mazazi matukufu ya mjukuu wake na muenezaji wa elimu yake Imam Swaadiq (a.s), atuenezee sisi sote fadhila zake zilizo pana na tawfiqi yake na wema wake duniani na akhera.
Kama ambavyo namuomba Mwenyezi Mungu mtukufu kumlinda na kumuhifadhi bwana wetu na kiongozi wetu Imam Mahdi (a.s) alie ahidiwa kuja Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake tukufu kwetu sote, kama ambavyo ninataraji kariimatu Ahlul-baiti mawlaatuna Fatima Maasumah (a.s) awe ni muombezi wetu katika haja zetu za duniani na akhera.
Amesema Mwenyezi Mungu mtukufu katika Qur’ani tukufu:

لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّهَ كَثِيراً

“ Bila shaka mnao mfano mwema kwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu, kwa mwenye kumuogopa Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, na kumtaja Mwenyeezi Mungu sana.”
(Suuratul-ahzaab aya 21)
Kisha mheshimiwa akasema: Maana tunayo faidika nayo kutoka kwenye aya hii tukufu ni kwamba Qur’an inatuamuru kujifunza au kuchukua kila kitu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na Aali zake (s.a.w.w), kwani wanazuoni wa elimu ya Balagha wanasema: (Kufutwa kwa kiambatanisho cha herufi ya jarri kunafaidisha kuwa hukumu ni ya ujumla).
Kwa hivyo basi someni Historia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na wekeni kando mambo yale ambayo yalikuwa yakihusika tu na ambayo yalikuwa mahsusi tu kwa Mtume (s.a.w.w) kama vile sala ya usiku ambayo ni wajibu kwake tu, na kuoa kwake wanawake tisa kwa ndoa ya daima, na kuingia kwake katika mji mtukufu wa Makka akiwa na silaha kwani kitendo hicho kiliruhusiwa kwake tu na mara moja tu na jambo hili halijuzu kwa yeyote mwinginewe tofauti na yeye kamwe.
Na pia someni na angalieni kwa makini ni kwa namna gani alikuwa akiamiliana na kuwatendea mateka wa vita, watumwa na watoto, waumini, waasi na wanafiki. Na ni namna gani alikuwa akitendeana na kuamiliana na mkewe na masahaba zake na watu wake wa karibu au ndugu zake, na ni vipi alikuwa akiamiliana na maadui zake na vipi alikuwa akiamiliana na mali yake binafsi na mali ya umma, na vipi alikuwa akiamiliana na Mwenyezi Mungu alie takasika.
Angalieni sira yake kwa makini na kwa kina kisha ifanyeni kuwa ni kigezo chenu, kwani kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu na kumfanya kigezo ni jambo la lazima kwa yule anae taka kufaulu na kuokoka katika Akhera kama alivyo sema Mwenyezi Mungu alie takasika: Kwa yule mwenye kumtaraji Mwenyezi Mungu na siku ya Akhera).
Na kuhusiana na sira na mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) mheshimiwa alisema: Nitakutajieni nukta mbili tu kuhusiana na sira ya Mtume mtukufu wa Mwenyezi Mungu na nitatosheka na kukomea kutaja mfano mmoja tu kuhusiana na kila nukta, kwa sababu mazungumzo kuhusiana na sira ya Mtume wa Mwenyezi Mungu yanahitaji mamia kadhaa ya masiku na nyusiku.


NUKTA YA KWANZA:
Kuto tetelekea kwake na kusimama kwake kidete (s.a.w.w).
Kwa hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa hateteleki na alikuwa madhubuti katika haki na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtukufu. Na kuna mifano mingi makumi kwa mamia juu ya ukweli huo na kati ya mifano hiyo ni huu ufuatao:
Pindi Mwenyezi Mungu alipo mpa Utume neno lake la kwanza (s.a.w.w) alilo zungumza na washirikina lilikuwa ni hili:

(قولوا لاإله إلا الله تفلحوا)

(Semeni Laailaha illa llahu mtaokoka).
Kutokana na ukweli kuwa washirikina walikuwa wakiabudu miungu mingi na ya aina tofauti kwani walikuwa na miungu iliyo tengenezwa kutokana na miti, pamba na chuma, na miungu ya mawe na udongo, na miungu iliyo tengenezwa kwa vitambaa Dhahabu na fedha na shaba, na kila kijiji kilikuwa na mungu wake maalum, na kila kabila lilikuwa na Mungu wake, na kila familia ilikuwa na Mungu wake maalum, na wakati mwingine kila mtu alikuwa na sanamu lake maalum, na kutokana na kuwa walikuwa wamekulia na kulelewa katika hali ya kuabudu masanamu kwa hivyo kauli hii ya Mtume (s.a.w.w) ilikuwa ni kubwa sana kwao.
Na iliwatatiza sana kauli hiyo na wakamjia Abu Twalib (a.s) baba mdogo wa Mtume (s.a.w.w) na wakamwambia: Hakika mtoto wa nduguyo amezidharau na kili zetu na njozi zetu na kuwaharibu vijana wetu …, basi mwambie ikiwa anatatizo la ufukara basi sisi tutamkusanyia mali imtoshelezayo kuwa tajiri sana kuliko waarabu wote na tutamfanya awe mfalme juu yetu, na wakataja mambo mengi kati ya mambo haya ya kutaka kumuhadaa. Na Abu Twalib akanukuu maneno yao na kumfahamisha Mtume (s.a.w.w) na Mtume alikuwa na uwezo wa kusema kuwa: Hii ni itikadi yangu, na ninazo dalili za kiakili ziwezazo kuyathibitisha hayo na ninaweza kumkinaisha yeyote atakae taka kujadiliana na mimi kuhusiana na ukweli kwamba Hakuna mola isipokuwa Mungu mmoja na kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa watu. Lakini Mtume (s.a.w.w) aliwajibu kwa maneno ambayo katika maneno hayo aliwazibia njia ziwezazo kuwafanya wamrudie tena kwa maneno mengine kwa mara ya pili kwani alisema: (Ewe ami yangu ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu hata kama wataliweka jua katika mkono wangu wa kulia na Mwezi kwenye mkono wangu wa kushoto ili niache jambo hili nisinge fanya hivyo kamwe).(Tafsiirul-qumiy juzu 2 \ Tafsiiru ya surat Swaad \ 228).
Huu ndio Umadhubuti na kuto teteleka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), na kila mwenye kuifahamu haki na kukinaika na haki hiyo basi ni juu yake kusimama kidete na kuwa imara kama kauli yake Mwenyezi Mungu isemavyo:

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ -13

(Hakika wale ambao wamesema Mola wetu ni Allah kisha wakasimama kidete bila kuteteleka basi watu hao hakuna khofu juu yao na wala hawata huzunika) (Suuratul-aqaaf aya 13) Basi ni juu yake kusimama kidete na madhubuti, lakini kusimama kidete kwa tabia na maadili mazuri, na si kwa kutumia nguvu na vitisho au ujabari.
Na akaongeza na kuendelea kusema: Na hebu tujifunze kusimama kidete kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na sisi tukiwa katika kumbu kumbu za kuzaliwa kwake kutukufu ni juu yetu kuazimia ndani ya nafsi zetu na nyoyo zetu na kufunga ahadi nae Mtume (s.a.w.w) ya kuwa tutasimama kidete na kuto teteleka, wakati huo tutakuwa tumepata bahati ya kupata dua yake na mambo yake (s.a.w.w) kwa sababu yeye anafahamu hivyo.
Kwa hivyo basi kila mtu ataulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu kuhusiana na yale anayo yaitakidi na kuyaaamini, na ataulizwa katika dunia mbele ya jamii yake na mbele ya wale watakao fikwa na habari zake na mbele ya historia katika siku za usoni.
Basi yule ambae anamuamini na kumuitakidi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ni juu yake kusimama kidete na kusimama madhubuti na kuto teteleka katika njia ya Mwenyezi Mungu, na yule ambae anamuamini Amiril-muuminiin na kumuitakidi ni juu yake kujizatiti na kuwa madhubuti katika njia ya Amiril-muuminiin (a.s) na yule anae muitakidi na kumuamini Fatima zahraa ni juu yake kusimama imara kwa ajili ya Fatima na katika njia yake (a.s), na yule ambae anamuitakidi na kumuamini Hasan na Huseini (a.s) ni juu yake kusimama kidete pamoja na maimamu hawa wawili juu yao rehma na amani, na yule ambae anawaitakidi maimamu wengine walio bakia ni juu yake kusimama imara na kuwa madhubuti pamoja nao (juu yao rehma na amani), na yule ambae amekinaika na kumuitakidi walii wa Mwenyezi Mungu mtukufu Swaahibul-asri waz-zamaan (Mwenye zama hizi) basi ni juu yake kusimama madhubuti pamoja nae (Ajjala llahu farajahush-sharifu) na kuto teteleka.

NUKTA YA PILI:
Tabia yake bora Mtume (s.a.w.w)
Ipekueni Historia na muiso kwa makini hadi mufahamu tabia na maadili matukufu ya Mtume, na kati yaliyo elezwa kwenye historia kama ifuatavyo: Pindi Mtume (s.a.w.w) alipokuwa katika mji wenye nuru wa Madina na wakati huo alikuwa ni mtawala na hakimu na raisi wa dola la kiislaam na kila kitu kilikuwa chini ya utawala wake na amri yake, alijiwa na ( Bedui mmoja na kulikamata juba lake na kulivuta kwa nguvu hadi (kutokana na kauli ya anasi anasema) niliangalia kwenye ncha ya shingo yake Mtume (s.a.w.w) na ikiwa imeathirika na kukwaruzika kwa kola ya juba lile kutokana na uvutaji ule wa nguvu kisha akamwambia Mtume: Ewe Muhammad amuru nipewe sehemu ya mali ya Mwenyezi Mungu ambayo unayo (iliyoko kwako).

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akamgeukia na kucheka na akaamuru apewe mali).(Makaarimul-akhlaaq\ katika unyenyekevu wake na maisha yake (s.a.w.w) ukurasa 17).
Yaani Mtume (s.a.w.w) alimsamehe na hakumtendea kama alivyo mtendea yeye. Na Mtume (s.a.w.w) alikuwa na uwezo wa kumlipishia na alikuwa na uwezo wa kumpiga bedui yule au kumuachia maswahaba wake au kuchukua kisasi kwake kwa sababu Mwenyezi Mungu mtukufu anasema:


فَمَنِ اعْتَدَى عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُواْ عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَى عَلَيْكُمْ وَاتَّقُواْ اللّهَ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ


“ Basi anae washambulieni, nanyi pia mumshambulie kwa kadiri alivyowashambulieni, na muogopeni mwenyeezi Mungu na jueni ya kwamba Mwenveezi Mungu yuko pamoia na wamchao.” (Suuratul-baqarah aya 194). Lakini Mtume (s.a.w.w) hakumlipizia kwa uovu bali alimtendea wema.
Sasa je katika dunia ya leo kuna raisi yeyote wa dola ambae kuna uwezekano wa kumkaribia na kumsogelea seuze kuvuta nguo yake?
Na Mtume (s.a.w.w) alikuwa na wake na baadhi yao walikuwa na muamala mbaya pamoja na Mtume (s.a.w.w) na kwa hakika Qur’an iliwakemea zaidi ya mara moja kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:


إِن تَتُوبَا إِلَى اللَّهِ فَقَدْ صَغَتْ قُلُوبُكُمَا وَإِن تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَلِكَ ظَهِيرٌ


Kama nyinyi wawili mtatubu kwa Mwenyeezi Mungu basi nyoyo zenu zimekwisha elekea upande, na kama mtasaidiana dhidi yake (Mtume) basi Mwenyeezi Mungu ni Mlinzi wake, na Jibril, na Waumini wema, na zaidi ya hayo (pia) Malaika ni wasaidizi (wake). (Suuratut-tahriim aya 4).
Bali mmoja wao alishitakia na kulalamikia kuhusiana na utume wake (s.a.w.w). Na kwa hakika riwaya zimetaja ya kuwa mwanamke huyo alimwambia Mtume (s.a.w.w): Wewe unadai ya kuwa ni mtume? Na hakuna yeyote alie nukuu ya kuwa mwanamke huyo aliamini na kuwa na yakini na utume wake hapo baadae.
Na pia imenukuliwa kuwa: Kulikuwa kati ya mwanamke huyo na kati ya Mtume (s.a.w.w) majibizano ya maneno na mwanamke huyo kumuingiza baba yake kama hakimu na muamuzi na akasema kumwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): Sema, na usisema isipokuwa kweli na haki, na baba yake mwanamke huyo kumpiga kofi na akasema: Ewe adui wa Mwenyezi Mungu! Mtume asiseme haki na kweli? (Siraatul-mustakiim\ cha Bayyadhiy\ juzu 3 \ Faslu fii ummish-shuruur\ ukurasa 165, pia angalia kitabu Al-ihyaau cha Ghazaliy).
Hatujakuta hata mara moja ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimlipizia yeyote kati ya wakeze alie mfanyia uovu nae kumfanyia uovu mfano wake au kumlipiazia kama alivyo mfanyia, sawa uovu huo uwe wa maneno au kitendo.
Kama ambavyo Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa na masahaba wengi sana na kati ya masahaba hao kulikuwa na walio kuwa wazuri sana tena sana, na muovu kati yao alikuwa ni muovu kweli kweli, bali baadhi yao walikuwa ni wanafiki kama

Qur’ani ilivyo eleza wazi kuhusu hilo kwani Mwenyezi Mungu anasema:


وَمِمَّنْ حَوْلَكُم مِّنَ الأَعْرَابِ مُنَافِقُونَ وَمِنْ أَهْلِ الْمَدِينَةِ مَرَدُواْ عَلَى النِّفَاقِ لاَ تَعْلَمُهُمْ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ سَنُعَذِّبُهُم مَّرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَى عَذَابٍ عَظِيمٍ


Na katika mabedui wanaokaa pembezoni mwenu kuna wanafiki, na katika wenyeji wa Madina (pia) wamebobea katika unafiki, huwajui, sisi tunawajua tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa. (Suuratut-tawbah aya 101).
Tafuteni katika historia na angalieni ni vipi Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiamiliana nao.
Na mheshimiwa akasisitiza kwa kusema: Kwa hivyo ni wajibu tujifunze kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) tabia hii na tumfanye kuwa kiongozi na muongozaji wetu na kumuiga na tufanye kama alivyo kuwa akifanya, na uovu au makosa tufanyiwayo na marafiki zetu ndugu zetu na majirani zetu na wengineo tuyakabili na kufanya kama alivyo kuwa akifanya mtawala wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).
Na hili linahitaji kuazimia, na mwenye kuazimia na kukata shauri Mwenyezi Mungu mtukufu atampa tawfiqi na kumfanya awe katika orodha yake Mwenyezi Mungu alie takasika ya watu waliokuwa wakifuata nyendo za Mtume wa Mwenyezi Mungu na akimfanya kuwa kigezo chake (s.a.w.w) na miongoni mwa watu walio ifanyisha kazi aya tukufu.
Kwa hivyo tawfiqi yoyote haipatikani bila ya kuazimia na kukata shauri.
Na akawaelekea wanafunzi wa kiafrika kwa hotuba yake na kusema:
Nyuma yenu kuna mamia na maelfu katika bara la Afrika, bara ambalo watu wake walio wengi wako huru au wako karibu kupata uhuru, basi jaribuni kufaidika na anga hilo la uhuru lililopo kwa kufikisha historia na sera ya Mtume wa Mwenyezi Mungu mwenye kuchaguliwa (Al-mustafa) (s.a.w.w) na Ahlil-baiti zake walio watwaharifu (a.s) na kuzifikisha kwa mamilionu haya ya watu.
Hakika asilimia tisini kwa mia 90% kati ya wananchi wa Afrika si waislaam au hawawafahamu Ahlul-baiti wa Mtume (a.s) lakini watu hao sio wenye kuwapinga na kuwachukia, na hata wale wenye taasubi na chuki walio wafuata wale walio oshwa na kusafisha mabongo ikiwa wataufahamu ukweli na picha ya kweli ya Mtume mtukufu na Ahlil-baiti wake (a.s) watabadilika na kugeuka.
Na huenda neno moja au kisa kimoja au msitari mmoja wenye ibara kamili waweza ukabadilisha historia nzima ya mwanadamu na maisha yake, kama ilivyo fanyika kwa mwanazuoni mmoja ambae hakuwa akiwafahamu Ahlul-baiti (a.s) na alisimamishwa na herufi ya jarri ambayo ni ( من) iliyoko kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:
(Mwenyezi Mungu amewaahidi…) na hicho ni kipande cha mwisho katika aya ya 29 ya suratul-fat’hi ambayo imetaja sifa za masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).
Mwanazuoni huyu alifanya mazingatio katika aya hii tukufu na kuifikiria kwa makini, na akafikiri na kufanya utafiti katika vitabu mbali mbali na hadithi na historia na kuipata haki na ukweli na kusimama kidete kwenye haki hiyo. Kiasi kwamba alitoka na faida kwamba maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) si wote wako kwenye haki na si wote mienendo yao iko sawa na kwamba si wote wenye kusamehewa, na si wote watakao pewa malipo mazuri kwa kufuatana kwao na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na kwa matendo yao waliyo yafanya kama sala funga na hija na…..
Na akasisitiza mheshimiwa Swaadiq kwa kusema: Nyinyi katika mustakabali na siku za usoni kwa utashi wa Mwenyezi Mungu mtukufu mtakuwa ni wawakilishi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na Ahlil-baiti wake watwaharifu, kwa hivyo basi ni juu yenu kufuata nyayo zao (juu yao rehma na amani) katika matendo na kauli, na ni juu yenu kutekleleza katika maisha yenu mfumo wa maisha ya Mtume (s.a.w.w), na jifunzeni kutoka kwake kuto teteleka na kuwa madhubuti katika itikadi zenu na tabia zake nzuri, kwani mamilioni ya watu wa Afrika wanasubiri muongozo na uongofu wa Mtume mtukufu wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kupitia kwenu na kwa sababu yenu, na wanasubiri muongozo wa Qur’an tukufu kupitia kwenu, na muongozo wa Ahlul-baiti wake (juu yao rehma na amani) kwa kupitia kalamu zenu ndimi zenu na mbinu na njia zenu, kwa hivyo basi msiwanyime na kuwaharamishia uongofu huo, na suala hili linahitaji kufanya kazi na kujifunza kwa makini na kwa kina, na kufanya kazi kwa kiwango kikubwa hadi muweze kufanikiwa na kupata tawfiqi ya kufaulu.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu alie takasika na mtukufu nasi tukiwa katika kumbu kumbu hizi mbili kubwa na tukufu za kuzaliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na kumbu kumbu ya kuzaliwa mjukuu wake Imam Swaadiq (a.s), atuwafikishe na atujaalie sisi sote kufuata sunna za Mtume mtukufu (s.a.w.w) na Ahlil-baiti wake watwaharifu na wema.
Waswalla llahu alaa Muhammad wa Aalihi twahiriin.