3-UTUME

 Mwenyezi Mungu alie takasika alipo muumba mwanadam, alimtakia mwanadam huyo saada na kheri katika Dunia na neema pia pepo katika Akhera na haya hayathibiti na kupatikana isipokuwa mwanadam huyu atakapo kuwa na mipango au program inayo kwenda sambamba na akili yake na maumbile yake na awe na mfumo unao wiana na roho yake na kiwiliwili chake, na program hiyo au mpango huo uziguse na kuyahusu mambo yote au mahitaji yote ya akili na maumbile, na uwe ni mfumo ulio kamili na wenye kukidhi matakwa  yote ya kiroho na kimwili, haiwezekani kuwekwa kanuni hiyona mtu mwingine isipokuwa na muumba wa huyu mwanadam mwenye ujuzi wa matakwa na mahitaji yote ya mwanadam na vitu avipendavyo.

Na kutokana na ukweli kuwa ni Mwenyezi Mungu alie mtakia mwanadam saada wakati alipo muumba, basi ilikuwa ni juu yake kuipanga program na kuuweka mpango huo unao zihusu na kuzigusa sehemu zote za mwanadam (kiroho na kimwili) na kuweka mfumo ulio kamili uwezao kumfikisha mwanadam kwenye saada hiyo, kisha mfumo na program hiyo kuituma na kuifikisha kwa watu kupitia kwenye mikono ya watu waaminifu kati ya viumbe wake na waja wake walio hifadhiwa na utendaji wa makosa au kukosea na kusahau na walio twahirishwa kutokana na aibu mbalimbali na madhambi, nao si wengine bali ni manabii na mitume.

Kwa msingi huo: Nabii ni mtu ambae Mwenyezi Mungu humtelemshia wahyi (humletea ufunuo kutoka kwake) kwa maana hiyo ni kuwa Nabii au Mtume hutoa habari kutoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu bila kuwepo kiunganishi cha kiumbe yeyote, na manabii wamegawanyika makundi mawili:

1- Nabiyyun mursal: (Nabii alie tumwa): Huyu ni yule Nabii alie tumwa kwa ajili ya kuwaokoa watu, kutoka kwenye kiza hadi kwenye nuru na kuwatoa kwenye batili hadi kwenye haki na kuwatoa kwenye mambo ya kupanga yasiyo na ukweli wala uhakika na kuwafikisha kwenye uhakika wa mambo, na kuwatoa kwenye ujinga na kuwafikisha kwenye elimu.

2-Nabiyyun ghayri mursali: (Nabii asie tumwa) Nae ni yule ambae hutelemshiwa wahyi kwa ajili yake mwenyewe na hakuamrishwa kufikisha hukumu kwa watu.

Na idadi ya mitume ni laki moja na ishirini na nne elfu (124000) na kati ya hao walio tumwa kufikisha hukumu kwa watu ni wachache.

Na Mtume wa kwanza ni Aadam (a.s) na wa mwisho wao ni Mohammad (s.a.w).

Na manabii walio tumwa kufikisha ujumbe wamegawanyika makundi mawili: 1- Ulul-azmi

2- Wasio Ulul-azmi.

Ulul-azmi: ni wale ambao walitumwa na Mwenyezi Mungu mtukufu katika ardhi hii kuanzia mashariki hadi magharibi na kwa watu wote, nao ni watano.

1-Ibrahiim (a.s).

2-Nuhu (a.s).

3-Mussa (a.s).

4-Issa (a.s).

5-Mohammad (s.a.w).

Na Mayahudi ni miongoni mwa wafuasi wa Mussa (a.s), Wakiristo ni miongoni mwa wafuasi wa Issa (a.s) na Waislaam ni wafuasi wa Mohammad (s.a.w).

Lakini Uislaam ulifuta Dini zote zilizo tangulia, kwa hivyo basi haijuzu kuendelea kufuata Dini hizi bali ni lazima kwa watu wote kufuata mafunzo ya Uislaam kama Mwenyezi Mungu mtukufu alivyo sema:

(ومن يبتغ غير الاسلام ديناً فلن يُقبل منه وهو في الآخرة من الخاسرين(1

Suratu aali-imraan aya /85.

Kwa hivyo basi Uyahudi na Ukiristo ni batili, na Uislaam unabakia kuwa ndio sheria ya Mwenyezi Mungu hadi siku ya kiama na haitafutwa kamwe milele na milele.

Na Mitume wasio ulul-azmi: ni wale ambao walitumwa na Mwenyezi Mungu mtukufu kwenye sehemu maalum na nchi fulani au sehemu fulani tu na kwa watu maalum.

 

MTUME WA MWISHO (S.A.W)

Hakika umekwisha fahamu ya kuwa Mohammad (s.a.w) ndie Mtume wa mwisho na kwamba dini yake- ambayo ni Uislaam- imefuta Dini zilizo tangulia na kwamba sheria yake itaendelea kuwepo na itabakia hadi siku ya kiama na kwamba ndio sheria pekee yenye uwezo wa kumfikisha mwanadamu kwenye saada na kuyathibitisha matarajio yake na matamanio yake katika maisha ya Dunia na Akhera kama ambavyo Mtume (s.a.w) ndie pekee ambae ni kigezo cha wanadamu na kigezo kilicho kamili katika upande wa kheri na mambo ya fadhili (ubora) kwa waislaam wote bali kwa ulimwengu wote ikiwa watajitakia kheri wao wenyewe, kwa kuifuata sera yake na kujipamba kwa tabia yake (s.a.w) na kuifahamu sehemu fulani ya historia yake (s.a.w) ni lazima kutaja baadhi ya sifa na mwenendo wake.[2] Yeye ni Mohammad bin Abdallah (s.a.w) na mama yake ni Aamina binti wahab.

Alizaliwa katika mji wa Makkatul mukarramah, siku ya ijumaa tarehe kumi na saba (17) mwezi wa Rabiiul-awwal (mfungo sita) baada ya kuchomoza Al-fajiri mwaka wa tembo katika zama za mfalme muadilifu [3](Kisraa)

 

KUPEWA UTUME KWA MTUKUFU MTUME (S.A.W)

Mtume (s.a.w) alipewa ujumbe wa kiislaam mnamo tarehe (27) mwezi wa Rajabul murajjab baada ya kutimiza miaka (40) katika umri wake mtukufu, kwani alishukiwa na jibrilu (a.s) ambae ni malaika mtukufu na alie karibu na Mwenyezi Mungu mtukufu na wakati huo Mtume (s.a.w) alikuwa katika pango la (Hiraa) nao ni mlima ulioko kwenye mji wa Makka na alitelemka kwake akiwa na aya tano za suratul Alaq kama zifuatazo:

بسم الله الرحمن الرحيم. اقرا باسم ربك الذي خلق. خلق الإنسان من علق. اقرا وربّك الآكرم. الّذي علّم بالقلم. علّم الإنسان مالم يعلم.(4)

Baada ya tukio hilo Mtume (s.a.w) alisimama kwenye mlima wa Swafa na katika masjidul-haraam na katika makundi ya watu na katika sehemu za makutanio ya watu, kwa ajili kufikisha ujumbe wa mola wake na kuwaita watu na kuwaongoza kwa Mwenyezi Mungu mtukufu na kumuamini huku akisema:

ياأيها الناس قولوا لا إلاإله إلا الله  تفلحوا.

Enyi watu semeni hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mungu mmoja mtafaulu.[5] Na kutokana na ukweli kuwa watu wa Makkah walikuwa ni washirikina na maraisi (viongozi) wao walikuwa wakiona maslahi yao binafsi yako kwenye shirki na kwa kuogopea maslahi yao wakawa wakimfanyia shere (wakimfanyia istihzaa na kumkebehi pia kumuudhi), na Mtume kila alivyo kuwa akiendelea na kazi yake ya wito wa kuwaongoza washirikina, pia wao waliendelea na kuzidisha maudhi yao kwa Mtume (s.a.w) mpaka akafikia hatua ya kusema:

(ما أوذي نبي مثل ما أوذ يت)

Hakuudhiwa Mtume yeyote kama nilivyo udhiwa mimi (au hakuna Mtume yeyote aliepata maudhi mfano wa maudhi niliyo yapata mimi).[6]

Na hawakumuamini isipokuwa watu wachache, wa kwanza wao akiwa Amirul muuminiin Ali bi Abi Twalib (a.s) na katika wanawake Khadijah binti Khuwailid (a.s).

Na pindi mashinikizo ya washirikina kwake yalipo kithiri akaamua kuhamia kwenye mji wa Madinah, na kuhama huko au hijira hiyo ndio mwanzo wa tarehe ya Waislaam.

Na huko ndiko Waislaam waliko ongezeka na kukithiri na nguvu yao kuongezeka, na kwa ubora wa wafunzo ya hali ya juu ya Mtume na kutokana na sheria ya Uislaam iliyo nyepesi na yenye hekima,  wakawa ni mifano bora kabisa katika tabia, maadili na utu, na wakawa ni mifano bora katika utamaduni na wakawa wananchi bora, na kutokana na mafunzo hayo wakawapita na kuzivuka au kuzipituka tamaduni zote za ulimwengu na Dini zote za mbinguni na zisizo za mbinguni.

Na Mtume (s.a.w) wakati akiwa katika mji wa Madinatul Munawwarah alitokewa na vita pia mapigano mbalimbali, na vita vyote hivyo vilikuwa ni vita vya kujihami na kujibu uchokozi wa Washirikina, Mayahudi na Wakristo waliyo kuwa wakiyaelekeza kwa Waislaam, na Mtume (s.a.w) katika vita vyote akiangalia sana upande wa amani, huruma, usamehevu na ubora (fadhila), kwa hivyo ndio maana utakuta kwamba walio uwawa kati ya pande mbili hizo Waislaam na Washirikina katika vita vyake vya kujihami ambavyo vilifikia Thamanini na zaidi hawakuwa zaidi ya elfu moja na mia nne (1400), kama historia zilivyo nukuu na kusajili kwenye kumbukumbu zake.

 

KUFARIKI KWAKE KWENYE KUSIKITISHA NA KUHUZUNISHA

Tangu Mtume (s.a.w) alipopewa utume rasmi na kukabidhiwa ujumbe wa kiislaam mpaka kufariki kwake na kuiaga kwake Dunia hii alikuwa akiungwa mkono na wahyi (ufunuo), na Aminul-wahyi Jibraaillu (a.s) alikuwa akishuka kwake akiwa na Qur’ani tukufu au akimletea Qur’ani tukufu kutoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu kidogo kidogo na katika matukio mbali mbali, hadi kitabu hiki adhiim kikakamilika katika muda wa miaka ishirini na tatu (23), na Mwenyezi Mungu akamuamuru kukikusanya na kukipanga kama kilivyo hivi sasa.

Ndio, Mtume (s.a.w) alikuwa akipangilia na kuiwekea nidham Dini ya Waislaam na Dunia yao, na alikuwa akiwafundisha kitabu na hekima na akiwabainishia kanuni za ibada na twaa (utiifu) na maingiliano kati yao na uwiano wa kijamii na siasa, uchumi na mengine mengi.

Na baada ya Dini kukamilika- kwa kumtawalisha Ali bin Abi Twalib (a.s) Amirul muuminiin na Imam wa wachamungu na khalifa wa Mtume (s.a.w) baada yake na hili kufanyika katika siku ya Ghadiir tarehe kumi na nane (18) ya mwezi wa Dhil-hajjil haraam katika mwaka wa hijja ya kuaga na kumshukia kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

(اليوم اكملت لكم د ينكم و اتممت عليكم نعمتي و رضيت لكم الآسلام د ينا-(7

Mtume (s.a.w) aliugua ogonjwa mdogo na wa kawaida tu, lakini maradhi au ugonjwa ule ukawa ukizidi na kuongezeka hadi kuaga Dunia na kurejea kwa mola wake tarehe ishirini na nane (28) ya mwezi wa Safar mwaka wa kumi na moja (11) hijiria na wasii wake pia khalifa wake baada yake kusimamia jukumu la kuandaa mazishi yake nae ni Amirul muuminiin Ali (a.s) na kumzika katika chumba chake kwenye mji mtukufu wa Madina mahala ambapo ndipo lilipo kaburi lake tukufu kwa hivi sasa.

Hakika Mtume (s.a.w) katika hali zake zote na katika maisha yake yote alikuwa ni mfano wa hali ya juu katika uaminifu, utakasifu wa moyo (ikhlaas), ukweli, utekelezaji wa ahadi, uzuri wa tabia, ukarimu, elimu, upole, usamehevu, ulain, ukarimu, ushujaa, uchamungu, zuhudi (kujiepusha na ladha au anasa za kidunia), unyenyekevu, na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Na alikuwa ni mwenye kusifika kwa uzuri wa maumbile ya kimwili na alikuwa ni mzuri: uzuri wenye kulingana na umbile lake na unao nasibiana na umbile hilo, uso wake ulikuwa ni wenye kumeremeta na wenye nuru sana kama mbalamwezi yenye kuangaza katika usiku wa ukamilifu wake, kama ambavyo moyo wake mtukufu na roho yake ya hali ya juu na kubwa vilikuwa vimefikia kileleni mwa ukamilifu wa kiroho, kama upatikanao kwenye tabia na maadili, na sira yake pia sunna au mienendo yake ni nyeupe yenye kutoa miali kama jua  lenye kuangaza katika nusu ya mchana.

Kwa sura ya ujumla, hakika Mtume (s.a.w) alikuwa amekusanya ubora wote na fadhila zote na alikuwa ndio mahala pa utukufu na ukarimu na kitongoji cha elimu, uadilifu, uchamungu na ubora, na alikuwa ndio ofisi ya mambo ya Dini na Dunia na Dunia na Akhera, hakutokea kuwepo  mfano wake kati ya walio tangulia na hata tokea mfano wake hadi milele.

Huyu ndie Mtume wa Waislaam na hii ndio Dini ya kiislaam, hakika Dini yake ni Dini bora kuliko Dini zote, na kitabu chake ni bora kuliko vitabu vyote, kwani ni kama vile Mwenyezi Mungu alivyo sema:

(لايأ تيه الباطل من بين يد يه ولا من خلفه تنزيل من حكيم حميد(8

Suratu fuswilat aya 42/.


[1]- Suratu Aal-imraan aya 85.

[2]- Kwa ajili ya ufafanuzi zaidi rejea kitabu ( Waliawwali marrat fii tariikhil- Adam, juzu ya 1-2 na kitabu (Baaqatun Atwiratun fii Ahwalil khatamin-nabiyyiin) na ( Swiraatul fawaha) pia (Mohammad (s.a.w) wal-qur’an) kilicho andikwa na ayatullahil- udhmaa Sayyid Mohammad Al-husseiny shiraziy (mwenyezi Mungu amtakase)

[3] -Yaani alie muadilifu kwa asilimia Fulani ukimlimganisha na mwingine.

[4]- Suratul-alaq aya 1-2

[5]- Al- manaaqib juzu ya 1/ 56,  sehemu isemayo Katika mahali alipo kutana na makafiri katika kitabu chake.

[6]- Kashful-ghumma: juzu ya 2/ 537, sehemu ya 4/ mlango wa 5.

[7]- Kashful ghumma: juzu ya 2/ 537, sehemu ya 4/ mlango wa 5, Suratul maidah aya ya 3.

[8] Suratu Fuswilat aya 42.