UIMAM

Na Uimam-kama walivyo uarifisha-ni uongozi wa jumla katika mambo ya Dini na Dunia, na uongozi huo (uraisi) unakuwa ni wa mtu mmojawapo kati ya watu akiwa ni naibu wa Mtume (s.a.w) na Uimam ni wajibu kuwepo kwa hukumu ya akili, kwa sababu Uimam ni (lutfu) huruma ya Mwenyezi Mungu, hakika sisi tunafahamu kwa yakini ya kuwa watu wanapo kuwa na Raisi mwenye kuwaongoza na kuwaelekeza watu na mwenye kusikilizwa na kutiiwa na anae chukua haki ya mwenye kudhulumiwa kutoka kwa dhalimu na kumzuwia dhalimu kufanya dhulma yake watu hao watakuwa karibu zaidi na maisha mema na saada, na watakuwa mbali zaidi na ufisadi na uovu. [1]

Na bahthi ya Uimam ni miongoni mwa bahthi zinazo fuatia bahthi ya Utume na ni matawi yake,  kwa sababu Uimam ni uendelezaji wa kazi ya Utume na kubakia kwake, na ni wajibu katika Uimam yote yaliyo wajibu kwenye Utume kama Ismah na utwaharifu, na kwamba ni lazima Imam ateuliwe na Mwenyezi Mungu mtukufu kwa Nasi (dalili ya wazi) na kumuainisha kwa jina, na kwa neno moja ni  kuwa Imam anashirikiana pamoja na Mtume katika kila kitu isipokuwa wahyi (ufunuo), kwani Imam hatelemshiwi wahyi.

Kwa hivyo basi: Kama ambavyo Mwenyezi Mungu mtukufu anavyo wateua na kuwachagua mitume na manabii vivyo hivyo maimam na mawasii wa Mtume na makhalifa wake.

Na kwa hakika alimuainisha na kumteulia Mtume wetu Mohammad (s.a.w) mawasii na makhalifa kumi na mbili (12) na hawa ndio maimam kumi na mbili walio mashuhuri kwa waislaam wote [2]  nao ni hawa wafuatao kwa utaratibu wao.

1-Imam Amirul muuminiin Ali bi Abi Twalib (a.s) mtoto wa ami yake Mtume (s.a.w) na mume wa binti yake Fatuma (a.s).

2-Imam Hassan bin Ali (a.s) na mama yake ni Fatuma binti Mohammad (s.a.w).

3-Imam shahidi Hussen bin Ali (a.s) na mama yake ni Fatuma bint Mohammad (s.a.w).

4-Imam Zainul aabidina: Ali bin Hussen (a.s).

5-Imam Baaqir (a.s): Mohammad bin Ali (a.s).

6-Imam Swaadiq: Jaafar bin Mohammad (a.s).

7-Imam Kaadhim: Mussa bin Jaafar (a.s).

8-Imam Ridhaa: Ali bin Mussa (a.s).

9-Imam Jawaad: Mohamma bin Ali (a.s).

10-Imam Al-hadiy: Ali bin Mohammad (a.s).

11-Imam Askariy: Hassan bin Ali (a.s).

12-Imam Mahdiy: Mohammad bin Hassan Al-qaaim  (atakae simama) na mwenye kungojewa (Mwenyezi Mungu aharakishe faraji yake na kudhihiri kwake), na hawa maimam ndio hoja wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe wote na makhalifa wa Mtume wake (s.a.w) walio barikiwa, nao wote wanatokana na nuru ya Mtume (s.a.w), na walikuwa kama Mtume (s.a.w) katika elimu, upole, na fadhila, zuhdi (kuitupamkono dunia), uadilifu, Ismah,tabia njema na tabia bora, na sifa zingine njema. Vipi wasiwe na sifa kama hizo? Ili hali wao ni makhalifa wake na mawasii wake na maimamu wake (viongozi) kwa viumbe wake na hoja za Mwenyezi Mungu juu ya viumbe (wanadamu) wote baada yake.

Na ufuatao ni muhtasari wa historia ya kila mmoja kati yao (a.s) na historia ya binti wa Mtume (s.a.w) mke wa wasii wa Mutme (s.a.w) Fatuma Zahraa (a.s).

 

BINTI WA MTUME FATIMA ZAHRAA (A.S)

Yeye ni Fatima Zahraa (a.s) baba yake ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) Mohammad bin Abdillah  na mama yake ni Sayyidah Mtukufu Khadijah (a.s) mama wa waumini na mumewe ni bwana na wasii wa Mtume Ali Amirul muuminiin na watoto wake pia wajukuu wake ni maimam watwaharifu (a.s).

Alizaliwa (a.s) tarehe (20) ya mwezi wa Jamaddul-akhir mwaka wa (45) tangu kuzaliwa Mtume (s.a.w) na alikufa shahidi akiwa ni mwenye kudhulumiwa tarehe 3 Jamaadul Aakhir [3] siku ya juma nne mwaka wa kumi (11) hijiria akiwa na umri wa miaka (18) katika umri wa kuchanua maua waridi (yaani katika umri wa ujana wake).

Na Amirul muuminiin ndie alie simamia suala la kuandaa mazishi yake na kumzika katika mji wa madina na kulificha kaburi lake kutokana na usia wake ikiwa ni hoja kutokana na dhuluma aliyo fanyiwa na haki yake iliyo porwa na kuchukuliwa kwa nguvu.

Na Fatima alikuwa kama baba yake katika ibada  na uchamungu na ubora na Zuhdi, na Mwenyezi Mungu aliteremsha aya kadhaa kuhusiana na hadhi yake (kuhusiana nae).[4]

Na Mtume (s.a.w) ndie alie muita kwa laqabu (jina mashuhuri) ya (Sayyidatu nisaail aalamiin) Mbora wa wanawake wa ulimwenguni, na kumuita kwa kunia ya Ummu abiiha (Mama wa baba yake) na alikuwa akimpenda sana na kumtukuza sana na kwa kiwango kikubwa, hata ilifikia hatua kwamba anapo ingia kwa Mtume humkaribisha na kusimama kwa heshima yake na kumkalisha mahala pake na pengine alikuwa akiibusu mikono yake na Mtume (s.a.w) alikuwa akisema: Hakika Mwenyezi Mungu anaridhia kwa maridhio ya Fatima na anachukia kwa kuchukia Fatima.[5]

Alimzalia Amirul muuminiin (a.s) watoto wafuatao: Imam Hassan (a.s) na Imam Hussen (a.s) na Muhsin (a.s) lakini Muhsin mimba yake ilitoka kabla ya muda wake kutokana na maudhi na masaibu yaliyo mfika mama yake, na Sayyidatu Zainab (a.s) na Sayyidah Ummu kuluthuum (a.s).

 

IMAMA WA KWANZA

IMAM AMIRUL MUUMINIIN (A.S)

Yeye ni Ali bin Abi Twalib (a.s) na mama yake ni Fatuma binti Asad (a.s) nae ni mtoto wa Ami yake Mtume wa Allah (s.a.w) na mume wa binti yake na wasii wake na khalifa wake kwa watu baada yake, Amirul muuminiin na baba wa maimam (a.s).

Alizaliwa ndani ya Kaaba tukufu katika mji wa Makkah, siku ya ijuma tarehe kumi na tatu (13) ya mwezi wa Rajab baada ya miaka thalathini (30) tangu kuzaliwa kwa Mtume (s.a.w) na alikufa shahidi usiku wa siku ya ijumaa katika msikiti wa Al-kufa katika mihrab, kwa upanga wa Ibnu Muljim Al-muradiy na bwana huyu alikuwa ni miongoni mwa Makhawariji– na ilikuwa ni tarehe kumi na tisa (19) ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na kukutana au kurejea kwa mola wake baada ya siku tatu tangu apate dharuba lile na alikufa shahidi katika usiku wa tarehe (21) akiwa na umri wa miaka sitini na tatu (63), na maimam wawili Hassan na Hussen (a.s) ndio walio simamia suala la mazishi yake na kumzika katika mji wa Najaful-ashraf mahala ambapo ndipo lilipo kaburi lake hivi leo na kulificha kaburi lake kutokana na usia wake (a.s), ili liwe katika amani kutokana na mashambulizi ya makhawariji na wenye kulitembelea kaburi lake wasiweze kulifikia na kunufaika kwa kufanya hivyo [6] kisha imam Swadiq (a.s) akalitambulisha kwa watu pia imam Kaadhim (a.s).

Na anazo fadhila na sifa nyingi sana na zisizo hesabika, hakika yeye alikuwa ndie mtu wa kwanza kumuamini Mtume (s.a.w) na hakumshirikisha Mwenyezi Mungu hata chembe na wala hakusujudia sanamu kamwe na kutokana na hilo ndio maana ikasemwa kuwa linapo tajwa jina lake yasemwe maneno yafuatayo:Karrama llahu wajhahu (yaani Mwenyezi Mungu autukuze uso wake) na ushindi katika vita ulikuwa umefungamanishwa na bendera yake katika vita vyote, mwenye kusimama madhubuti na asie kimbia vitani, hakugeuka nyuma katika vita na wala hakukimbia kamwe na kutokana na hukumu zake nzuri ( au uzuri wa utoaji wa hukumu wa Ali Mtume akasema kuhusia nae: اقضاكم علي (Hakimu bora zaidi kati yenu ni Ali).[7] Na kutokana na wingi wa elimu yake Mtume (s.a.w) akasema: أنا مد ينة العلم وعلي بابها (Mimi ni jiji la elimu na Ali ni mlango wake).[8] na kutokana na kushikamana kwake na haki Mtume akasema: (علي مع الحق والحق مع علي) (Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali).[9]

Na alikuwa ni muadilifu kwa watu wake, akitoa haki kwa sawa, mwenye kujiepusha na mali za  kidunia, na alikuwa akija na kuingia kwenye hazina ya Waislaam (Baytul mali) na kuziangalia Dhahabu na Fedha na kusema:(يا صفراء ويا بيضاء غري غيري) (Ewe mwenye rangi ya  manjano (Dhahabu) na ewe mwenye rangi nyeupe (Fedha) mghuri (mdanganye) mwingine tofauti na mimi).[10] Kisha kuzitawanya kwa watu na habakishi hata tembe moja, na alikuwa akiwahurumia masikini na akikaa pamoja na mafukara na kukidhi haja za watu na akizungumza maneno ya haki na kweli na kuhukumu kwa uadilifu na kuhukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu.

Na alikuwa akitekeleza hukumu za Mwenyuezi Mungu, na akifuata mwenendo wa Mtume wa Allah (s.a.w) mpaka kheri ikaenea sehemu zote na baraka kutangaa na maisha bora na yenye neema (mazuri) kuwaenea   waja wote na katika miji yote.

Kwa ufupi ni kuwa: Yeye (a.s) alikuwa kama Mtume (s.a.w) katika sifa zote na mambo yote, isipokuwa katika suala la Wahyi na Utume na kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu akamfanya katika aya ya maapizano  (Mubahala) sawa na nafsi ya Mtume (s.a.w).[11]

 

IMAM WA PILI: IMAM MUJTABA (A.S)

Yeye ni Haassan bin Ali (a.s) bin Abi Twalib, na mama yake ni Fatima Zahraa (a.s) binti Mohammad (s.a.w) nae ni mjukuu mkubwa wa Mtume (s.a.w) na ni khalifa wake wa pili na Imam wa watu baada ya baba yake Amirul muuminiin (a.s).

Amezaliwa katika mji wa Madinatul munawwarah siku ya juma nne katikati ya mwezi wa Ramadhan mwaka wa tatu wa hijiria, na alikufa shahidi kwa sumu ambayo alitegeshewa na Muawia bin Abi Sufyaan kupitia mkewe Imam Hassan ambae ni Juudah binti Ash'ath na  hilo lilifanyika siku ya Al-khamisi tarehe saba (7) ya mwezi wa Safar [12] mwaka wa (50) hijiria, na alisimamia mazishi yake ndugu yake Imam Hussen (a.s) na kumsitiri katika makaburi ya Bakii’i katika mji wa Madinatul munawwarah, mahala ambapo ndipo kilipo kiwiliwili chake kwa hivi sasa  (ndipo mahala lilipo kaburi lake) na-kwa masikitiko makubwa- kaburi lake lilivunjwa na Mawahabi pia walivunja kuba la kaburi lake hilo.

Na Imam Hassan (a.s) alikuwa ni mfanya ibada kwa wingi kati ya watu wa zama zake na alikuwa ni mwenye elimu zaidi na mbora na alikuwa ni mwenye kumfanana sana Mtume (s.a.w), na alikuwa ni mkarimu zaidi kati ya Ahlul bayti wake katika zama zake na alikuwa ni mwenye huruma zaidi.

Na miongoni mwa ukarimu wake (a.s) ni kuwa alipewa mafuta uzuri na mjakazi mmoja wapo kati ya vijakazi wake, akasema kumwambia mjakazi yule: Wewe uko huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha akasema: Hivi ndivyo alivyo tuadabisha Mwenyezi Mungu pale alipo sema: واذا حييتم بتحية فحيوا بأحسن منها او رد واها) ) (Mnapo amkiwa kwa maamkizi basi itikieni kwa maamkizi mazuri zaidi kuliko mliyo amkiwa au rudisheni kwa yale maamkizi mliyo amkuliwa).[13]

Na miongoni mwa upole wake (a.s) ni kuwa mtu mmoja wa Sham alimuona akiwa amepanda mnyama, yule bwana akawa akimlaani Imam na Imam hakumjibu kwa chochote, yule bwana alipo maliza kutoa laana zake na matusi yake Imam Hassan akamwendea na kusema: Ewe shekh nadhani ni mgeni na huenda umenifananisha, lau unge omba tukuridhishe basi tunge kuridhisha, na lau kama unge tuomba kitu fulani tunge kupatia na lau kama unge taka tukuongoze tunge kuongoza na lau unge tutaka tukubebee mzigo wako tunge kubebea na ikiwa unanjaa tunge kushibisha na kama unge kuwa uchi tunge kuvisha na kama ni muhitaji tutakutajirisha na ikiwa umefukuzwa tutakuhifadhi na kukusitiri na ikiwa unahaja tutaitatua haja yako.[14]

Yule bwana alipo sikia maneno yale alilia na kusema: Nina shuhudia ya kuwa wewe ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika Ardhi yake, hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kufahamu vema mahala pa kuuweka ujumbe wake.

 

IMAM WA TATU: IMAM SHAHIID (A.S)

Yeye ni Hussen bin Ali bin Abi Twalib (a.s) na mama yake ni Fatima binti Mohammad (s.a.w) nae ni mjukuu wa Mtume (s.a.w) na Khalifa wake wa tatu na baba wa maimam tisa walio kuja baada yake na ni Imam wa watu baada ya nduguye au kaka yake Hassan (a.s).

Alizaliwa katika mji wa Madinatul-munawwarah tarehe tatu (3) ya mwezi wa Shaaban mwaka wa nne hijiria na kuuwawa kwa dhulma kwa upanga hali ya kuwa ni mwenye kiu, mauaji yaliyo fanya na bani Umayyah kwa amri ya Yazid bin Muawia katika tukio mashuhuri la Ashura, siku ya juma mosi tarehe kumi (10) ya mwezi wa Muharram mwaka (61) hijiria, na jeneza lake  pia kiwiliwili chake kitwaharifu  na kilicho katwa katwa kwa mapanga pamoja na viwiliwili vingine vya mashahidi walio kufa mashahid pamoja nae vilizikwa baada ya siku tatu tangu kuuwawa kwao wakiwa mashahidi na alaie mzika ni mwanae Imam Zainul aabidiin (a.s) na kumzika mahala ambapo ndipo kaburi lake lilipo hivi sasa katika mji mtukufu wa Karbalaa, mji ambao uliangukia mikononi mwa Saddam na kundi lake na Mwenyezi Mungu kuukomboa kutoka mikononi mwao-pamoja na sehemu zingine tukufu zilizoko Iraq.

Na fadhila zake ni nyingi sana kiasi kwamba ni vigumu kuweza kuzitaja zote, kwani yeye ni ua zuri la Mtume (s.a.w) ambae Mtume alisema kuhusiana na yeye: حسين مني وانا من حسين Hussein anatokana na mimi na mimi natokana na Hussen.[15]

Na pia amesema kuhusiana nae na kuhusu nduguye Hassan (a.s):

 هم ريحانتياي من الد نيا          

 (Wao wawili ni maua yangu mazuri duniani).[16]

Pia amesema (s.a.w):الحسن والحسين سيدا شباب اهل الجنة

Hassan na Hussedin ni mabwana wa vijana wa peponi.[17]

Pia amesema (s.a.w):

الحسن والحسين إمامان قاما أو قعدا [18]

 Hassan na Hussein ni maimam sawa wakiwa wamesimam au wamekaa.

Na alikuwa ni mwenye elimu zaidi na mfanya ibada sana kati ya watu, hakika alikuwa akisali kila usiku rakaa elfu moja kama baba yake Amirul muuminiin (a.s) na mara nyingi alikuwa akibeba mfuko wa ngozi wenye vyakula usiku na kuwapelekea mafakiri hadi ilionekana alama na athari yake mgongoni mwake baada ya kuuliwa na alikuwa ni mkarimu, mtukufu, mpole, na alikuwa mkali sana pindi anapo asiwa Mwenyezi Mungu.

Na miongoni mwa ukarimu wake ni pale alipojiwa na bedui mmoja akimuomba na kumuimbia shairi lisemalo: Hakwenda kombo kwa hivi sasa mwenye kukuelekea kwa matarajio na alie bisha mlangoni kwa mara kadhaa, wewe ni mkarimu na wewe ni mwenye kutegemewa, baba yako alikuwa ni muuaji wa mafasiki, lau kama si yule ambae alikuwa mwanzoni mwenu, basi sisi sote tunge enewa na kuzungukwa na  moto wa jahannama.

Imam Hussen akampatia dinari elfu nne na akmuomba msamaha kwa kusema: Zichukue hakika mimi nakuomba samahani na fahamu ya kuwa mimi ni mwenye huruma sana kwako, lau kama mwendo wetu kesho ungekuwa ni mwema, na anga letu lingekumiminia kheri nyingi, lakini matatizo ya zama ni ya aina tofauti na yenye kubadilika kwa hivyo na mkono wangu  ni wenye kutoa kidogo.

Na kwa hakika Imam (a.s) kwa kisimamo chake cha kishujaa-na ambacho hakina mfano katika ulimwengu-aliweza kuihuisha sheria ya kiislaam na dini ya babu yake Mtume (s.a.w) bali aliuhuisha ulimwengu wote hadi siku ya kiama, kwa hivyo yeye ni bwana wa mashahidi na ni mtu bora baada ya kaka yake na nduguye Hassan (a.s).

 

IMAM WA NNE: IMAMA SAJJAD (A.S)

Yeye ni Imam Ali bin Hussen (a.s) na mama yake ni Shahri banuu binti wa mfalme Yazdjard na Imam huyu (a.s) alikuwa akiitwa Mtoto wa wateule wawili, kutokana na kauli ya Mtume (s.a.w): Hakika mwenyezi Mungu ana wateule wawili katika waja wake, mteule wake katika waarabu ni Quraishi na katika waajemi (wasio waarabu) ni ni Mfursi na kwa kuyazingatia maana ya maneno haya Abul Aswad akaimba shairi lifuatalo: Hakika mtoto alie zaliwa kati ya Kisraa na Haashim ni mkarimu zaidi ya watoto wote walio vishwa hirizi shingoni mwao.

Amezaliwa (a.s) katika mji wa Madinanatul-munawwarah siku ya Ali-khamisi mwezi mtukufu wa Shaaban [19] mwaka (38) hijiria na kufa shahidi kwa sumu siku ya juma mosi tarehe (25) mwezi wa Muharram [20] mwaka (95) akiwa na umri wa miaka (57), na mwanae Imam Baaqir (a.s) ndie alie simamia suala la mazishi yake na kumzika karibu na kaburi la Ami yake Imam Mujtaba (a.s) katika mji wa madinatul-munawwarah.

Na alikuwa ni wa aina yake (kwa maana ya kuwa hakuwa na mfano) katika zama zake katika suala la elimu, ibada, fadhila, uchamungu, kuwasaidia watu wenye kuomba misaada na wenye kutaka usaidizi na mengineyo, na maulamaa wengi pia mafaqihi wamepokea riwaya nyingi sana na zisizo hesabika  kutoka kwake na kuhifadhi kutoka kwake dua na mawaidha mengi na karama mbalimbali na mengine mengi yasiyo hesabika.

Na alikuwa akitoka usiku wa kiza na kubeba mfuko mabegani mwake ukiwa na Dinari na Dirham napengine alikuwa akibeba mgongoni mwake mfuko wa vyakula, au kuni na kupita mlango mmoja mmoja akibisha hodi na kumpatia kila atokae kwenye nyumba hizo pesa hizo, na alikuwa akifunika kichwa chake ili mafakiri wasimfahamu, na pindi alipo fariki watu wa madina wakafahamu na kuelewa ya kuwa yeye (a.s) ndie ambae alikuwa akibeba mfuko na kuwapatia vyakula.

Pamoja na hayo akipendezewa sana kula pamoja na mafukara au kuhudhuria kwenye chaku chake mayatima na mafakiri na kula pamoja nae.

Na miongoni mwa tabia zake njema (a.s) ni kuwa katika kila mwezi alikuwa akiwaita wahudumu wake na kusema: Mwenye kutaka kuolewa kati yanu nitamuoza, au akitaka kuuzwa nitamuuza, au akitaka kuachiwa huru nitamuachia huru.

Na pindi alipokuwa akijiwa na muombaji husema: Karibu wewe ambae huibeba akiba yangu ya akhera.

Na kutokana na uchaji mwingi wa mola ni kuwa alikuwa akisali kwa usiku na mcana wake rakaa elfu mmoja na anapo kuwa kwenye sala ngozi yake husinyaa na kukunjamana na rangi yake kubadilika na kuwa ya njano na kutetemeka kama kuti la mtende, na miongoni mwa laqabu zake ni Dhuthafanaati (mwenye sugu au magamba), kutokana na athari za sajda katika paji lake la uso na vitanga vyake pia magotini mwake.

Mtu mmoja alimtusi na kumtolea maneno machafu na mabaya na yeye (a.s) akiwa kimia hazungumzi wala kasema chochote na baada ya muda Imam (a.s) akamwendea, waliokuwa wamehudhuria wakadhania ya kuwa anataka kumfanya kama alivyo fanya yeye, mara akasoma aya ifuatayo:

والكاظمين الغيظ والعافين عن الناس والله يحب المحسنين)[21]

Na wenye kuvunja ghadhabu na kuwasamehe watu na Mwenyezi Mungu anawapenda watu wema.

Kisha akamsimamia bwana yule na kusema: Ewe ndugu yangu hakika wewe ulisimama kwangu (ulinisimamia) muda ulio pita na kusema uliyo yasema, ikiwa umeyasema kwangu hayo uliyo yasema, basi mimi nina muomba Mwenyezi Mungu msamaha na ikiwa umesema mambo ambayo siko nayo, Mwenyezi Mungu akusamehe. [22]

 

IMAM WA TANO: IMAM BAAQIR (A.S)

Yeye ni Imam Mohammad bin Ali Al-baaqir (a.s) na mama yake ni Fatuma binti Hassan (a.s) alizaliwa katika mji wa madina siku ya Ijumaa mwanzoni mwa mwezi mtukufu wa Rajab [23] mwaka (57) hijiria. Na yeye ndie mtu wa kwanza katika kizazi cha Ali alie zaliwa na wazazi wawili watokanao na kizazi hicho cha Ali, na ni mtu wa kwanza wa kizazi cha Haashim alie zaliwa na wazazi wawili watokanao na kizazi cha Haashim, na ni mtu wa kwanza alie zaliwa na wazazi wawili watokanao na kizazi cha Fatuma, kwani yeye ndie wa mwanzo alie kusanya kati ya kizazi cha maimamu wawili Hassana na Hussen (a.s) na alikufa shahidi kwa sumu siku ya juma tatu tarehe (7) Dhul hajjil haraam mwaka (114) hijiria akiwa na umri wa miaka (57) na mwanae Imam Swaadiq (a.s) ndie alie simamia suala la maandalizi ya  mazishi yake na kumzika pembezoni mwa kaburi la baba yake Imam Sajjad (a.s) na Ami wa baba yake na babu yake Imam Mujtaba (a.s) katika makaburi ya Baqii'i kwenye mji wa Madinatuil munawwarah.

Na alikuwa ni mwenye fadhila kubwa mkarimu na mwenye kushikamana na dini na alikuwa ni mwenye elimu nyingi na kubwa na mpole sana, pia mwenye tabia njema na mwenye kufanya ibada sana, mwenye unyenyekevu, ukarimu, ukunjufu na alifikia kwenye kilele katika tabia zake njema, mkiristo mmoja alimwambia: Wewe ni mfunguzi na mpasuaji!

Imam akasema: Mimi ni Mfuinguzi.

Akasema wewe ni mtoto wa mpishi.

Imam akasema: Hiyo ni kazi yake.

Akasema: Wewe ni mtoto wa mtu mweusi na mbaya.

Imam (a.s) akasema: Ikiwa umesema kweli Mwenyezi Mungu amsamehe na ikiwa umesema uongo Mwenyezi Mungu akusamehe.

Yule Mkiristo akasilimu.

Na katika elimu alikuwa kama Bahari yenye mawimbi mengi, akijibu kila mas'ala na swali lolote analo ulizwa bila kusita. Na Ibnu Atwaa Al-makiy amesema: Sija wahi kuona kamwe wanazuoni na maulamaa kwa mtu yeyote alie kuwa mdogo zaidi kuliko nilivyo waona kwa Baaqir (a.s) hakika nilimuona Al-hakam bin Utaybah-pamoja na utukufu wake na heshima yake kati ya watu-akiwa mbele yake kama mtoto akiwa mbele ya mwalimu wake, na Mohammad bin Muslim amesema: Sikujiwa na fikra yoyote isipokuwa nilimuuliza Mohammad bin Ali (a.s) mpaka nilimuuliza hadithi elifu thalathini (30).

Na Imam (a.s) alikuwa ni mwenye kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wakati wote, mpaka Imam Swaadiq (a.s) akasema: Baba yangu alikuwa ni mwenye kumtaja sana Mwenyezi Mungu, nilikuwa nikitembea pamoja nae hali ya kuwa akimtaja Mwenyezi Mungu na alikuwa akizungumza na watu  na lisimshughulishe hilo kunako kumtaja Mwenyezi Mungu. [24]

Na Imam alikuwa ni mwingi wa tahajjud (sala za usiku) na ibada, mwenye kulia sana na mwenye mazingatio.

 

IMAM WA SITA: IMAM SWAADIQ (A.S)

Yeye ni Jaafar bin Mohammad As-swaadiq (a.s) na mama yake ni Fatuma alie kuwa akiitwa kwa kunia ya (Ummu farwah) alizaliwa (a.s) katika mji wa Madinatul-munawwarah siku ya Ijumaa tarehe (17) mwezi wa Rabiiul Aawwal (mfungo sita) siku ya kuzaliwa Mtume (s.a.w) mwaka (83) hijiria na kufa shahidi kwa sumu siku ya juma nne tarehe (25) mwezi wa Shawwal (mfungo mosi) mwaka (148) hijiria  akiwa na umri wa miaka (65), na mwanae Imam Kaadhim kusimamia maandalizi ya mazishi yake na kumzika katika makaburi ya Baqii'i pembezoni mwa kaburi la baba yake Imam Baaqir (a.s) na babu zake wawili: Imam Sajjad na Imam Mujtaba (a.s).

Na alikuwa na Fadhila nyingi zisizo hesabika kama elimu, fadhila, hekima, fiqhi, zuhdi, uchamungu, ukweli, uadilifu, ubora, furaha na utoaji, ukarimu, ushujaa na fadhila zinginezo.

Na kwa hakika Mufiid alisema (Mwenyezi mungu autukuze utajo wake): Na maulamaa hawakunukuu kwa yeyote kati ya Ahlul bayti wake kama walivyo nukuu kutoka kwake na hakuna yeyote kati ya watu wakusanyao hadithi na wakusanyaji wa habari, mfano wa Jaafar bin Mohammad As-swaadiq (a.s) hakika walikusanya majina ya wapokezi kutoka kwake kati ya watu waaminifu pamoja na kutofautiana kwao kirai na itikadi, na walikuwa ni watu elfu nne (4000) [25] …. Hadi mwisho wa maneno yake.

Na Abu hanifa Imamu wa madhehebu ya hanafi alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wake moja kwa moja, kama ambavyo maimam wengine wa madhehebu za Ahli sunna walikuwa ni wa wanafunzi wake pia (a.s) lakini si moja kwa moja bali kwa kupitia wanafunzi wake na kwamba elimu nyingi na mpya kama vile Kemia, Fizikia na elimu ya maumbo na nyota na elimu ya ugunduzi wa madini na kuchimbuaji wa hazina zilizoko ardhini na zinginezo nyingi ambazo Imam ndie alie weka misingi yake na kuwaongoza watu kwenye elimu hizo.

Hakika Imam (a.s) alitumia fursa iliyopatikana ya ugomvi kati ya bani Abbas walio fanya mapinduzi dhidi ya bani Umayyah na kati ya bani umayya walio kuwa mbioni kuanguka na kutoweka dola lao, alitumia fursa hiyo kuanzisha Madrasa kubwa ya kielimu na kujishughulisha na kazi ya ulezi wa wanafunzi na watafutaji wa elimu na kuwabainishia mafunzo ya kiislaam na uzuri wa sheria zake na kuwafafanulia fikra za batili na mbaya zilizo ingia kwenye Uislaam na kubatilisha shubha zitolewazo, mpaka misingi ya sheria ikaimarika na ubainifu wa Uislaam kudhihiri na kubainika wazi na akafahamika (a.s) kama Raisi na kiongozi wa Madhehebu ya Jaafaria, kama ambavyo wafuasi wake (a.s) walifahamika pia kwa jina la Shiatu Jaafar (wafuasi wa Jaafar au mashia wa Jaafar).

Na miongoni mwa uongofu wake (a.s) ni kuwa yeye alikuwa akila siki na mafuta na kuvaa kanzu ngumu na nzito napengine alikuwa akivaa nguo yenye viraka na alikuwa akifanya kazi zake mwenyewe kwenmye mabustani na mashamba yake.

Na miongoni mwa Ibada zake ni kuwa alikuwa akisali sana  na pengine alikuwa akizimia katika sala na kuitwa watu wa kumsaidia usiku, Mtumishi wake anasema: Nilikwenda mlangoni kwake na nikamkuta katika chumba chake cha faragha akiwa ameweka shavu lake juu ya udongo hali akiomba kwa kuinua vitanga vyake na huku kukiwa na athari ya mchanga usoni mwake na kwenye shavu lake.  

Na Imam (a.s) alikuwa ni mwingi wa kutoa, mwenye tabia njema, mwenye maneno laini, mwenye vikao vizuri na mwenye bashasha kwa kila mwenye kukutana nae na alikuwa na muashara mzuri kwa kila anae kutana nae.

 

IMAM WA SABA: IMAM KAADHIM (A.S)

Yeye ni Imam Mussa bin Jaafar Al-kaadhim (a.s) na mama yake ni Hamidah Al-muswaffah, alizaliwa (a.s) katika sehemu iitwayo (Ab’waa) nayo ni sehemu iliyoko kati ya Makka na Madina siku ya juma pili tarehe (7) mwezi wa Safar mwaka (128) hijiria na aliiaga Dunia akiwa na umri wa miaka (55) kwa kulishwa Sumu na kufa shahidi katika jela ya Haroun baada ya kumfunga kwa muda mrefu kwa muda wa miaka (14) kwa dhuluma na uadui, na alifariki siku ya Ijumaa tarehe (25) ya mwezi wa Rajab mwaka (183) na mwanae Imam Ridhaa (a.s) kusimamia maandalizi ya mazishi yake na kumzika mahala lilipo kaburi lake tukufu kwa hivi sasa katika mji wa Kaadhimiyyah huko Iraq.

Na Imam alikuwa ndie mwenye elumu zaidi kati ya watu wa zama zake na mbora wao na mkarimu zaidi kati yao na shujaa zaidi na amwenye tabia njema, mwenye umbile bora na mororo, mwenye kudhihiri juu yake fadhila, elimu na mwenye hadhi tukufu, mwenye kufanya sana ibada na mwenye kurefusha sijda zake, na kutokana na kuvunja kwake ghadhabu na kuto kasirika akaitwa Al-kaadhim, na kutokana na wema wake na utukufu wake alikuwa akiitwa Al-abdus swalih (mja mwema).

Na kutokana na elimu yake nyingi aliweza kudhihirisha elimu za aina tofauti, elimu ambazo ziliwashangaza watu, na kati ya elimu hizo ni hadithi ya (Burayha) [26] mkuu wa Wakiristo alie mashuhuri alie shindwa na Imam na kukosa la kusema mwishowe kusilimu na kuwa muislaam safi.

Na miongoni mwa ukarimu wake (a.s) ni kuwa fakiri mmoja alimuomba Dinari mia moja  na Imam kwa kutaka kumjaribu akamuuliza mas'ala au swali moja ili kujua kiwango cha maarifa yake, yule fakiri alipo jibu mas'ala yale Imam akampatia Dinari elfu moja.

Na Imam (a.s) alikuwa ni mwenye sauti nzuri sana pindi anapo soma Qur'ani na alikuwa ni mfanya ibada sana kati ya watu na kusoma sana Qur'ani, na alikuwa ni mwenye kurefusha sana sijda na rukuu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na mwenye kulia sana na mwenye mazingatio, na alifikiwa na shahada hali ya kuwa yuko kwenye hali ya kusujudu (yaani akiwa ni mmwenye kusujudu).

 

IMAM WA NANE: IMAM RIDHAA (A.S)

Yeye ni Imam Ali bin Mussa Ridhaa (a.s) na mama yake ni Sayyidah Najmah, alizaliwa (a.s) siku ya Al-khamisi tarehe (11) mwezi wa Dhulqaadatul-haraam, mwaka (148) hijiria katika mji wa Madina na kufa shahidi kwa sumu siku ya Ijumaa mwishoni mwa mwezi wa Safar, mwaka (203) na mwanae Imam Jawaad (a.s) kusimamia suala la maandalizi ya mazishi yake na kumzika katika sehemu ya khorasani sehemu ambayo ndiko liliko kaburi lake tukufu.

Na Imam (a.s) alikuwa mashuhuri sana kwa elimu nyingi, fadhila, ukarimu, mwingi wa kutoa, mwenye tabia njema, mnyenyekevu, na mwenye kufanya ibada sana.

Maamun-kutokana na vitimbi na hadaa-alimuita Imam Ridhaa (a.s) kutoka Madinah hadi Khorasani (Iran) na kumtaka achukue ukhalifa wa kiislaam-badala yake-lakini Imam alikuwa amejiweka kando na kuyapa mgongo  mambo ya kidunia (yaani alikuwa ni mwenye zuhdi) na hakukubali, kwani alifahamu matokeo ya maombi hayo, kuwa ni vitimbi na hadaa, kama ambavyo babu yake Amirul muuminiin (a.s) alivyo kataa Ukhalifa-katika shura-wakati Ibnu Auf alipo mpatia Ukhalifa huo kwa sharti kwamba afuate sera ya mashekhe wawili walio mtangulia, (Abubakar na Omar), kwani Imam aliona ya kuwa Ukhalifa wakati huo ulikuwa umesimama juu ya jambo moja wapo kati ya mambo mawili, na mambo yote mawili hayo ni ya uongo na si yenye kukubaliwa na kuridhiwa na Mwenyezi Mungu mtukufu: Ama jambo la kwanza ni kuwa Imam (a.s) akubali sharti kisha asilitekeleze-kama alivyo fanya Othumani-na huo ni uongo wa kikauli na wenye kuchukiwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Ama jambo la pili ni kuwa: Imam akubali sharti na atekeleze, maana yake ni kuwa aridhie sera ya mashekhe wawili pamoja na kuwa hakuwa na ridhaa na hakuridhishwa na matendo yao na huo ni uongo wa kimatendo na ni wenye kukemewa mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa hivyo basi Imam hakuona njia yenye kuridhiwa na Mwenyezi Mungu tofauti na kukataa na kupinga na kuto kubali.[27]

Na baada ya Imam Ridhaa (a.s) kuukataa Ukhalifa, Maamun alishikwa na butwaa na kunyongea sana kwani aliona ya kuwa mpango wake ambao kwa ajili yake alimuita Imam umeshindwa na kufeli, hapo alimtaka achukue wilayatul ahad -cheo cha waziri mkuu- na kumlazimisha kukubali (a.s) lakini Imam (a.s) alimuwekea sharti ya kuwa hato ingilia katika jambo lolote kati ya mambo ya dola na kukubali cheo hicho kwa sharti hilo.

Imam (a.s) alikuwa ni mrithi wa baba zake watukufu (a.s) katika elimu na babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) na elimu yake ilionekana na kudhihiri kiasi kidogo kuhusiana na mambo ya dini na Madhehebu  fikra na Itikadi-katika kikao cha majadiliano ambacho kiliandaliwa na Maamuun-na yaliyo jitokeza kwenye hadithi ya Rukbaan.

Vile vile katika ibada alikuwa (a.s) akikesha katika masiku mengi kwa ibada na kuhitimisha Qur'ani kwa muda wa siku tatu na mara nyingi alikuwa akisali usiku na mchana rakaa elfu moja, na mara nyingi alikuwa akisujudu kwa muda mrefu, pengine alichukua masaa kadhaa kwenye sijda na alikuwa ni mwengi wa kufunga.

Na Imam (a.s) alikuwa ni mwingi wa kutenda mema, na akitoa sana sadaka na sadaka nyingi alikuwa kizitoa kwa siri na hasa kwenye usiku wa kiza.

Na miongoni mwa tabia zake na adabu zake (a.s) ni kuwa hakumuudhi mtu yeyote kwa maneno kamwe na wala hakumfanyia ukali mtu yeyote katika kauli, na hakuwa akiegemea kukiwa kuna watu wamekaa mbele yake na hakuwahi kucheka kwa sauti kubwa na ya juu kamwe, na hakuwahi kutema mate mbele ya yeyote kamwe, na chakula kilipo kuwa tayari mezani huwaita ahli zake wote na wahudumu wake na kula pamoja nao.

 

IMAM WA TISA: IMAM JAWAAD (A.S)

Yeye ni Imam Mohammad bin Ali Al-jawaad (a.s) na mama yake ni Sayyidah Sabiika, alizaliwa (a.s) siku ya Ijumaa tarehe (10) katika mwezi mtukufu wa Rajab, mwaka (195) hijiria, katika mji wa Madinatul munawwarah na kufa shahidi kwa sumu katika mji wa Baghdaad, mwishoni mwa mwezi wa Dhul-qaadah (mfungo pili) mwaka (220) hijiria, na mwanae Imam Al-hadiy (a.s) kusimamia maandalizi ya mazishi yake na kumzika kwenye maburi ya Makuraishi pembezoni mwa kaburi la babu yake Muusa bin Jaafar (a.s) katika mji wa Kaadhimiyyah mahala lilipo kaburi lake kwa hivi sasa.

Na Imam (a.s) alikuwa ni mjuzi zaidi kati ya watu wa zama zake na mbora zaidi kuliko watu wote, mkarimu, pia mwingi wa kutoa na mwenye vikao vizuri, na alikuwa ni mwenye tabia njema, mfasaha na kila alipo kuwa akipanda mnyama wake hubeba Dhahabu na Fedha na hakuna aliekuwa akimuomba isipokuwa humpatia, na alie kuwa akimuomba pamoja na wingi wao alikuwa hampatiii chini ya Dinari Khamsini (50) na alie kuwa akimuomba kati ya shangazi zake alikuwa hampi chini ya Dinari ishirini na tano (25). 

Na miongoni mwa elimu yake kubwa ambayo ilidhihiri kwa watu: Ni kuwa wanazuoni thamanini kati ya wanazuoni wa miji mbalimbali walikusanyika kwake baada ya kurudi kwao kutoka kwenye ibada ya hijja na kumuuliza kuhusiana na mas'ala mbali mbali na yeye (a.s) kuwajibu, namiongoni mwa mambo ya ajabu yaliyo simuliwa kutoka kwake (a.s) ni kuwa watu wengi walikusanyika kwake na kumuuliza mas'ala thelethini elfu-katika kikao kimoja nacho ni kikao kiitwacho kwa siku hizi kwa jina la kongamamno, kongamano ambalo  hufanyika na kuendelea kwa muda wa  siku kadhaa na Imam kuwajibu mas'ala hayo bila kusita kufanya hivyo wala kukosea na wakati huo akiwa na umri wa miaka tisa (9), lakini jambo kama hili si jambo la ajabu na la kushangaza kutokea kwa Ahlul bayti-watu wa nyumba ya Wahyi na mahala alipokuwa Jibril (a.s) akitelemka akiwa na  Qur'ani na hasa baada ya Qur'ani kuzungumzia kuhusiana na kupewa kwa Issa bin Maryam kitabu na Utume hali ya kuwa bado yuko kwenye kitanda chake akiwa mtoto mchanga.

Kisha ni kuwa khalifa Alimuoza binti yake na hilo lilifanyika baada ya kumtahini kwa maswali (mas'ala) muhimu na kuyajibu yote-katika kisa mashuhuri-.

 

IMAMA WA KUMI: IMAM AL-HADIY (A.S) 

Yeye ni Imam Ali bin Mohammad Al-hadiy (a.s) mama yake ni Sayyidah Samanah.

Alizaliwa (a.s) katika mji wa Madinatul-munawwarah siku ya Ijumaa tarehe (2) mwezi mtukufu wa Rajab, mwaka (212) hijiria na kufa shahidi kwa sumu kwenye mji wa Samarraa siku ya juma tatu tarehe (3) mwezi wa Rajab, mwaka (254) hijiria, na mwanae Imam Askariy (a.s) kusimamia maandalizi ya mazishi yake, na kumzika ndani ya nyumba yake kwenye mji wa Samarraa mahala lilipo kaburi lake kwa hivi sasa na mahala kilipo lazwa kiwili wili chake kitukufu.

Na Imam (a.s) alikuwa ni mtu bora kati ya watu wa zama zake na alikuwa ni mwenye elimu zaidi na alie kusanya fadhila zote na mkarimu sana na mwingi wa kutoa na alikuwa ni mwenye maneno laini na aliekuwa akimuabudu sana Mwenyezi Mungu na mwenye sera nzuri nasafi na mwenye tabia njema.

Na miongoni mwa ukarimu wake ni kisa kilicho pokelewa na (Ardabiliy) katika kisa chake ya kuwa: Khalifa alimtumia Dirham elfu thalathini, Imam akampatia bedui mmoja wa Al-kufa kama zawadi na akamwambia: Toa kiasi ulipe madeni yako na kiasi kitakacho bakia kitumie kwa ajili ya matumizi na mahitaji ya familia yako na ahali zako na utusamehe.

Yule bedui akamwambia Imam: Ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu hakika deni nililo kuwa nalo halifikii theluthi ya pesa hii. (Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kufahamu vema mahala pakuuweka ujumbe wake), na akachukua pesa zile na kwenda zake.[28]

 

IMAM WA KUMI NA MOJA: IMAM ASKARIY (A.S)

Yeye ni Imam Hassan bin Ali Al-askariy (a.s) na mama yake ni Sayyidah Hadiitha.

Alizaliwa katika mji wa Madinatul-munawwarah siku ya Ijumaa tarhe nane (8) mwezi wa Rabiul-aakhir, na inasemekana kuwa amezaliwa tarehe kumi na mbili (12) Rabiul-aakhir [29] mwaka (232) hijiria na kufa shahidi kwa Sumu siku ya Ijumaa tarehe nane (8) mwezi wa Rabiul-awwal mwaka (206) hijiria, na mwanae Imam Hujjatul-muntadhar (mwenye kungojewa) ndie alie simamia maandalizi ya mazishi yake na kumzika karibu na kaburi la baba yake Imam Al-hadiy (a.s) katika mji wa Samarra, mahala ambapo ndipo lilipo kaburi lake kwa hivi sasa.

Na Imam (a.s) alikuwa ni mfano wa juu kabisa katika ubora, elimu, utoaji, sharafu, furaha na ukarimu, ibada, unyenyekevu na tabia zingine nyingi njema, na alikuwa ni mfano wa kuigwa na kigezo chema kwa wengine, na alikuwa ni mwenye urefu wa wastani na mzuri wa umbile, mwenye uso mzuri na kiwiliwili cha wastani, mwenye heshima na hadhi kubwa kwenye nyoyo na mwenye nafasi ya juu na tukufu katika nafsi za watu, na Imam (a.s) alikuwa akimfanana sana babu yake Mtume (s.a.w) katika tabia zake na mwendo wake mwema na uzuri wa kuishi vema na watu.

 Na miongoni mwa visa vya ukarimu wake ni kisa kilicho pokelewa na Ismail kisemacho: Nilimkalia na kumsubiri Imam (a.s) katikati ya njia, alipo fika na kupita mahala nilipo kuwa nikamueleza ufukara wangu. Imam akasema (a.s): Unaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwa uongo kwani umefukia Dinari miambili  chini ya Ardhi na kusema kwangu maneno haya si kwa sababu ya kuto taka kukupa, ewe ghulam (Mhudumu) mpatie ulicho nacho, akasema: Yule mhudumu akanipatia Dinari mia moja.[30]

Na kuna mtu mwingine alimwendea Imam-alipo sikia ukunjufu wake na ukarimu wake-na alikuwa akihitaji Dirhamu mia tano, Imam (a.s) akampatia Dirham mia tano na kumuongezea Dirhamu zingine mia tatu.[31]

Na kwa hakika watu wote walitoa ushahidi na kuthibitisha ubora wake na ukarimu wake, hata wakiristo walimshuhudia (a.s) ya kuwa yeye anafanana na masihi (Yesu) katika ubora, elimu, ukarimu na miujiza yake, na Imam (a.s) alikuwa ni mwenye kufanya sana ibada, akisali sala za usiku (tahajjud) daiama na alikuwa ni mwenye mandhari ya wema, na mwenye heba kubwa.

 

IMAM WA KUMI NA MBILI: IMAM AL-MUNTADHAR (A.S)

(Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake)

Yeye ndie Imam na Al-hujjatul-mahdiy (a.s), Mohammad bin Hassan (a.s) na mama yake ni Sayyidah Narjis.

Alizaliwa (a.s) katika mji wa Samarraa usiku wa nusu ya mwezi wa Shaaban, mwaka (255) hijiria.

Na yeye (a.s) ndio hoja wa mwisho wa Mwenyezi Mungu juu ya ardhi na Khalifa wa mwisho wa Mtume (s.a.w) na Imam wa mwisho wa Waislaam, maimam ambao ni kumi na mbili na Mwenyezi Mungu-kwa utashi wake-ameurefusha umri wake mtukufu katika Dunia hii ili ardhi isibakie bila hujja wa Mwenyezi Mungu, kwani kama kusinge kuwa na hujja basi ardhi inge didimia pamoja na watu wake na yeye Imam haonekani kwa watu na Mwenyezi Mungu atamdhihirisha katika Aakhiriz-zamani (Zama za mwisho) baada ya Dunia kujawa na dhuluma na ujeuri (uovu), ili aijaze dunia hiyo kwa uadilifu na usawa.

Hakika Mtume (s.a.w) na maimam watwaharifu walitoa habari ya kuwa yeye atakuwa na ghaibah (Atatoweka na kuto onekana) kwa muda mrefu, na hatakuwa thabiti kwenye juu ya Uimam na wilaya yake na kumuamini isipokuwa yule ambae Mwenyezi Mungu ameujaribu moyo wake kwa Imani, na katika siku za ghaiba yake atakuwa katika hali ya kuwafikishia manufaa watu wa Ardhini kama jua lifikishavyo manufaa na faida zake kwa watu hao hata kama litakuwa limefunikwa na mawingu, na Mwenyezi Mungu atambakiza hai mpaka utakapo fika wakati wa kudhihiri kwake, na hapo kudhihiri kwa idhini yake Mwenyezi Mungu mtukufu na kuimiliki (kuitawala) Dunia yote na kueneza uadilifu na usawa Duniani na kueneza Uislaam na misingi yake yote na kuitekeleza Qur'ani na amri zake kwa watu wote na katika nyanja zake zote za maisha, na hapo Kheri kuenea na saada kutangaa kwenye  miji yote na kuwaenea waja wote na kuthibitika kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo:

[32]  ليظهره علي الدين كله ولو كره المشركون)

Ili auidhihirishe Uislaam juu ya dini zote hata kuma washirikina watachukia.

Ewe Mwenyezi Mungu harakisha faraja yake na kufanye kwepesi kudhihiri  kwake na utujaalie tuwe miongoni mwa wasaidizi na answari wake.

Baada ya hayo  ni jambo lililo wazi ya kuwa Imam Al-mahdiy (a.s) alipokuja kuandaa mazishi ya baba yake Imam As-kariy (a.s) na kumsalia watawala waovu walifahamu kuwepo kwa mrithi na mshika nafasi baada ya Imam Askariy (a.s) na hili lili waogopesha sana juu ya utawala wao na wakafikiria njia ya kumkamata na kumuua kama walivyo waua baba zake (a.s) ili kwa kufanya hivyo waokoke na kujinusuru na habari zilizo wafikia  kutoka kwa Mtume (s.a.w) kuhusiana na habari za Imam wa kumi na mbili na kwamba yeye ndie ambae atakae maliza na kuangamiza utawala wa waovu na kuchukua utawala huo, na Imam Mahdiy (a.s) alikuwa ameamuriwa na Mwenyezi Mungu mtukufu kuwa kwenye ghaiba na kuto onekana kwa watu.

Na pindi majasusi wa Khalifa walipo muona na kuivamia nyumba yake akaghibu na kutoweka na kuto onekana kwa watu na kufichika kunako macho yao, na hilo lilifanyika kwa Imam kutokea kwenye mlango mwingine ulio kuwa wazi wenye kutokea kwenye Sirdab (nyumba ya chini) iliyo kuwa na mlango wa kutokea nje bila yeyote kati yao kumuona, na kutokana na ukweli kwamba sehemu ambayo ilikuwa ndio mahala pa kughibu kwake ni nyumba yake (a.s) Waislaam wakaifanya ile sehemu inasibishwayo kwake-katika mji wa Samarra-iliyo mashuhuri kuwa ni sirdab ya kughibu kwake, wakaifanya kuwa msikiti na mahala pa kufanyia ziara (kutembelea).


[1] Na inawezekana kuiffafanua kwa kutoa mfano ufuatao: nao ni kwamba chi ya Iraq na Japan baada ya vita vya pili vya dunia, chi hizi mbili zilikuwa katika msitari mmoja wa uharibifu na ubomozi na kurudi nyuma kimaendeleo, na kuto songa mbele kimaendeleo, lakini Japan baada ya muda kadhaa iliweza kuwa sawa bali kuzipita kwa kiwango kikubwa nchi na madola makubwa ya magharibi katika fani mbali mbali na katika viwanda, maendeleo na kushamiri kwake, wakati ambapo Iraq ilibakia ikiwa ni yenye kuharibika na kurudi nyuma kimaendeleo ikiwa masikini mwenye kuhitaji, ikiingiza kila kitu kutoka nje ya nchi hata ngano na nyama na hata nyuzi za kushonea na sindano, na wataalam pia wachambuzi wa mambo walio toa sababu na illa ya tofauti kati ya nchi mbili hizo ya kuwa viongozi wan chi ya Japan walikuwa ni wenye uwezo wa kuongoza na viongozi walio iongoza Iraq hawakuwa na uwezo wa kustahili kuongoza, haya ni katika upande wa kimadda, ama kwa upande wa kimaanawia pia ni jambo lililo wazi, kwa hivyo katika hadithi tukufu isemayo: (من لا معاش له لا معاد له)  (asie kuwa na maisha hana marejeo) inamaanisha kuwa: Ufukara wa duniani ni hasara katika Akhera, ukionhezea na mengine yaliyo pokelewa kutoka kwa Fatuma Zahraa (a.s) ya kuwa amesema: Lau kama wasinge upora ukhalifa, dunia wa watu ing kuwa njema na yenye neema na Akhera yao pia na kusinge kuwa na tofauti tofauti kati ya watu wawili.

[2] Akiashiria kwenye kauli yake Mtume (s.a.w) isemayo:

الخلفاء من بعدي اثنا عشر    (Makhalifa baada yangu ni kumi na mbili)

Na hadithi hii ni (Muttafaqun alyhi) yaani maulamaa wamewafikiana juu ya usahihi wake na ni mashuhuri kati ya waislaam wote Sunnah na Shia. Rejea kwenye kitabu Al-khiswal: ukurasa 478, hadithi ya 43, Makhalifa na maimamu naada ya Mtume (s.a.w), pia kitabu Al-irshaad: Mujallad wa 2/ 345 mlango Majaalis fin nassi….., Kashful ghummah: Mujallad wa 2/ 447, mlango wa Maa jaa’a minan-nassi………, Aalaamul waraa: Ukurasa 396 sehemu ya pili, Kitabu saliim bin Qaysi: Ukurasa 141 na rejea Sihahus- sittaza Ahli sunna. 

[3] Inasemekana ya kuwa kufariki kwake ilikuwa ni baada ya siku 75 tanfu kufariki kwa Mtume (s.a.w) na inasemekana ilikuwa ni baada ya siku 95 tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w).

[4] Rejea kwenye kitabu: ( Fatwimatuz-zahraa fil qur’ani) cha Ayatullahil udhmaa Sayyid Swaadiq Shiraziy (Mwnyezi Mungu amhifadhi

[5] Rejea kitabu Ihtijaaj ukurasa 354, mahojiano ya Abi Abdillahi (a.s) na katika majadiliano hayo kuna maneno yafuatayo: ya kuwa Mtume (s.a.w) alimwambia Fatuma: (Ewe Fatuma hakika mwenyezi Mungu anachukia kwa kuchukia kwako na anaridhia kwa kuridhia kwako).

[6] Kwa sababu Hajjaj- kama ilivyo nukuliwa kwenye historia ua kuwa alifukua makaburi laki moja akitafuta kaburi lake (a.s).

[7] Kasful ghumma: Mujaalad wa 1/ 263, na Al-ihtijaaj: Ukurasa 391.

[8]Al-aamaaly cha Shekh Swaadiq: Ukurasa 345, majlis ya Khamsini na tano (55).  

[9] Al-jamal: ukurasa  81 na Al-fusuulul mukhtaar: Ukurasa 97.

[10] Al-manaaqib: Mujallad wa 3/ 257 katika sehemu izungumziayo: Fii musawaatihi ma’a Daud wa Twaluut wa Sulaiman (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake).

[11] Suratu Al-imaraan aya 61.

[12] Na inasemekana kuwa ni Safar 28.

[13] Suratun-nisaa aya 86.

[14] Al-manaaqib: Mujallad wa 4/ 19 sehemu ya Makaarimul-Akhlaaq.

[15] Al-irshaad: Mujallad wa 2/ 127, mlango wa Twarafun min fadhaailil-hussein (a.s).

[16] Al-manaaqib: Mujallad wa 4/ 76, sehemu ya Fii ma’aali Umurihi. Na kuna riwaya kutoka kwa Ibnu Omar isemayo: Nilimsikia (s.a.w) akisema:

الحسن والحسين ريحانتاي في الد نيا.

[17] Al-aamaliy cha Shekh Swaduuq: Ukurasa 57, hadithi ya 10.

[18] Ilalush-sharaai’I: Ukurasa 211, hadithi ya 2, mlango wa Al-illatullatiy min ajliha swaalahal hassan bin Ali (a.s).

[19] Na inasemekana ya kuwa: Mwaka w tano mwezi wa Shaaban.

[20] Na inasemekana ya kuwa ni tarehe 12 au 18 ya mwezi wa Muharram.

[21] Suratu Al- Imraan aya 134.

[22] Aalamul-waraa: Ukurasa 216, sehemu ya nne: Fii dhikri baadhi mu’ujizaatihi wa manaaqibihi wa Fadhaailihi.

[23] Na inasemekana kuwa ni: Tarehe mosi Mwezi wa Rajab.

[24] Uddatud-daiy: Ukurasa 248, mlango wa tano: Fiima Ulhiqa bidduaa wahuwa Adhikri.

[25] Na inasemekana ni Elfu ishirini.

[26] Attawhiid: Ukurasa 27, mlango wa Arrad alaa lladhiina qaalu Inna llah thaalithu.

[27] Rejea Nahjul balagha: Sharhu ya Ibnu Abil hadiid: Mujallad wa 1/ 188 kisa cha shuraa.

[28] Kashful- ghumma: Mujallad wa 2/374, Dhikru Imamul Aashir Abil Hassan Ali (a.s).

[29] Na inasemekana ni wa:  nane.

[30] Al-irshaad: Mujallad wa 2/332, mlango wa Dhikru Twarafun min Akhbaar Abi Mohammad

[31] - Al-irshaad: Mujallad wa 2/326, mlango wa Dhikru Twarafun min Akhbaar Abi Mohammad.

[32]-Suratu-tawbah aya 33.